“Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye hata malaika walio mbinguni wala mwana ila Baba peke yake.” Siku Hiyo ya Kiama


Siku Hiyo ya Kiama

Husema kujifutua, kwa hino yao huduma,
Maneno yao huzua, ili wapewe hishima,
Hutaka tukatambua, tuwakabidhi adhama,
Hakuna anayejua, siku hiyo ya kiama!

Siku itakopotua, ajuaye ni Karima,
Watawaza kuwazua, siku wasijue vema,
Hakuna wa kung’amua, akabashiri kusema,
Hakuna anayejua, siku hiyo ya kiama!

Waja hujifaragua, kwa kubashiri daima,
Matokeo hurajua, lakini yote hukwama,
Bure watajifunua, uchao wakalalama,
Hakuna anayejua, siku hiyo ya kiama!

Hata mkaomba dua, mtabaki tu mwaguma,
Mzidi kujishaua, hukumu itaandama,
Ubashiri kuzidua, kwa hizo zenu taluma,
Hakuna anayejua, siku hiyo ya kiama!

Tangazo nalikagua, lao hilo linavuma,
Mungu ndiye hutatua, mwanadamu huungama,
Siku yake tateua, bila nabii kutuma,
Hakuna anayejua, siku hiyo ya kiama!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*