Kupanda mchongoma kushuka ndio ngoma. Mchongoma ni mti wenye mimba ambao upandwa kama ua mwisho wa shamba. Ukiupanda uingie shamba la mtu ili ufuate matunda fulani basi wakati shuka na kuondoka utadungwa na mimba mpaka utajutia kitendo cha kupanda. Kuupanda Mchongoma


Kuupanda Mchongoma

Wa miiba waupanda, juu yake mchongoma,
Kula matunda waenda, huhisi ikijitoma,
Haya yote wayatenda, ujuapo wenda pema,
Kuupanda mchongoma, na kushuka ndiko ngoma.

Watumbukia kizani, peke yako kujitoma,
Wajikalisha pembeni, na pasiwe kuloloma,
Kishaye tabu waghani, usemapo zakuchoma,
Kuupanda mchongoma, na kushuka ndiko ngoma.

Wapenda ushirikina, ndio upate neema,
Badala ya Maulana, kwao wachawi wanema,
Pendavyo ushirikina, wakatisha ghanima,
Kuupanda mchongoma, na kushuka ndiko ngoma.

Watumbukia tegoni, utafutapo neema,
Wapapatika mwishoni, upatapo umezama,
Jiepushe mitegoni, usipojitoa hima,
Kuupanda mchongoma, na kushuka ndiko ngoma.

Hatimaye wanong’ona, na kujitwika lawama,
Hamu ndiyo huna tena, ya kupanda mchongoma,
Sasa hisi huna tena, miiba ilojitoma,
Kuupanda mchongoma, na kushuka ndiko ngoma.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*