Usimcheke kilema! Si kutaka wala kupenda kwake. Uonapo u mzima shukuru Mungu. Hujui linalokusubiri. Afya ni majaliwa ya Mungu! Mcheka Kilema


Mcheka Kilema

Silika yangu wacheka, hunioni mahashumu,
Ufyonzi watukutika, yote kwa kutaamamu,
Wanitundika mahoka, nisiye nazo timamu,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Sikani kwa udhilifu, upungufu wa akili,
Busara yangu dhaifu, legevu yangu tamuli,
Matendo ya ukashifu, ni kwa hii yangu hali,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Nyota kutano kichwano, taka za kipilipili,
Vazi upurukushani, laonyesha yangu hali,
Uchafuko kusakini, abadi kwa azali,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kutwaa taka sokoni, na fumba kuibebea,
Uhaji ni upindani, shabuko lakuotea,
Shambulio ni usani litendalo kunyendea,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Wanicheka unadhifu, kutenga wangu urari,
Wauona ukashifu, ubashiri kuhadhiri,
Wanicheka uvunjifu, wajiona kushamiri,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kutuzi ni shambulio, ulio wa ufukuto,
Mwakumbatia kimbio, la kuume kwa kushoto,
Ganjo lao kimbilio, vinionapo vitoto,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kila mara mwalipuka, vishindo vya kishetani,
Uhali wangu mwacheka, udadisi wa utani,
Pale pole napozuka, nawapata wapindani,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Ni leo ti mwanicheka, keshoi wenu waumbuka,
Kesho yenu ni uzuka, licha ya kuvivinyuka,
Kichaa nacho ukoka, kitambacho kwa hakika,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Huo wenu ni upofu, hatimaye usoona,
Enyi ndio wapunjufu, walio na uhiana,
Wana wa uharibifu, na wema mkijiona,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*