Mwanadamu hawezi kuchungwa kama kondoo. Ana yake mengi ya kufanya angaa apate riziki yake. Mwache atarazaki! Achungwaye ni Ng’onzi


Achungwaye ni Ng’onzi

Endapo utanichunga, unichunge kwa werevu,
Unichunge nikipanga, mipango yenye uchovu,
Unanifanya mjinga, achana na yangu kovu,
Kuchunga ungenichunga, ningekuwa wako ng’onzi.

Niwinge nikiwa kuku, nisile wako mtama,
Utazame kila siku, nd’o unitie lawama,
Wasikiza ya wadaku, Ili unipe shutuma,
Mpaka ifike siku ile kubwa ya Karima,-
Kuchunga ungenichunga, ningekuwa wako ng’onzi.

Lolote wataka ‘jua, unichunge nifanyayo,
Kijificha wachemua, nami kagundua hayo,
Siku hizi nimekua, usinifuate nyayo,
Nami nitaomba dua, aniepushiye hayo,
Kuchunga ungenichunga, ningekuwa wako ng’onzi.

Muda ndio wapoteza, usemapo wanichunga,
Hadi usiku wa kiza, kwangu kote utatanga,
Ujue ninachouza, nd’o maana wanichunga,
Kamtafute ajuza, mzee wa kumchunga,
Kuchunga ungenichunga, ningekuwa wako ng’onzi.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*