Gazeti la Taifa Leo nchini Kenya limekuwa katika mstari wa kwanza kukuza Kiswahili na kuwapa motisha washairi chipukizi. Hili hapa shairi la kusifia gazeti hilo. Napongeza Taifa Leo


Napongeza Taifa Leo

Nahakiki mwanong’ona, na kubekua barani,
Tarafetu karakana, tanuu ya siasani,
Jogoo wengi baina, najitokeza msani,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Siasa kwanza nakana, edita napongezeni,
Ubingwa wenu wafana usokuwa nuksani,
Katu sio ya hiana, kojangu nawavikeni,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Molangu namlingana, kumkabidhi sukani,
Abadi uwe mtana, azali kiswahilini,
Taifa leo dafina, toka bara hadi pwani,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Nikusomapo kwa inna, adangu huwa jubuni,
Watunzi wa kulumbana, raha yao ja legeni,
Wasanii wako shina, wakuchorao katuni,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Cha ghiliba ndicho sina, sifa njema sikuhini,
Kukirihi ndiko huna, tahaririyo laini,
Daima wapirikana, nakupa yangu nishani,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana,

Tangu kusuhubiana, kwangu ni kama jibini,
Ufasaha kwa upana, kanipakia wazoni,
Lugha nayo kupambana, na kulimbuka msani,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

La faragha nalinena, nakukalisha makani,
Barua zaandamana, yu mchache kurasani,
Nyingi za kuambatana, Lughetu tuikuzeni,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Uhondo kwanza nabana, ninao mwingi junguni,
Naghubika kwa kiana, natia nanga jukwani,
Tumshukuru Rabana, sote tulo ukumbini,
Taifa Leo nchini, napongeza kwa upana.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*