Wapo baadhi wa watu wenye sifa tele. Pesa hawana ila ni matajiri wa sifa na umaarufu. “Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.” Swifa Zako si Adimu

Swifa Zako si Adimu

Naabtadi awamu, wasifu hadi pomoni,
Nakupenda madhulumu, subirazo maidani,
Staha waikadimu, nakshi yako tungoni,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Ushopoapo nudhumu, twajitenga faraghani,
Twakujuwa mahashumu, u mweledi wa amani,
Huna bee wala mimu, japo u mwinyi bongoni,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Huna zako darahimu, yamekukepa mapeni,
Umejaliwa ghanimu, ukabaki u laini,
Megubikwa ukarimu, taadhima huighani,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Umepambwa uharimu, kukomaa ukubwani,
Vema umestakimu, utepetevu  hunani,
Muhali wakutuhumu, dhahiri wamebaini,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Weledi wamezuumu, kukujua kwa undani,
Busara waifahamu, ustawi kutamani,
Imefifia dhulamu, hupenda kutamakani,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*