Wanaopayuka huudhi mno. Watasema chochote bila kujali wala kuchunguza. Huwa ndio asili ya lolote linalosemwa bila kujali. “Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!” Kupayuka Kwanongesha


Kupayuka Kwanongesha

Kukanya yangu faradhi, maonyo yatakutosha,
Sitishwi na yako hadhi, sharuti mie kupasha,
Majukumu hujakidhi, hutanga ukapotosha,
Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!

Nakupa wangu waadhi, ukome kudodosesha,
Hikuhusu yangu hodhi, wengine kuwaonesha,
Kitwani una maradhi, bongoni yanakuwasha,
Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!

Hunayo njema mbawadhi, kutwa takuaibisha,
Wajibandika ukadhi, watu kuwanyamazisha,
Kwa wazee huna radhi, mila’zo kutaabisha,
Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!

Imekuwa yako kodhi, kujua na kujulisha,
Kajifanya mfawidhi, baraza kulikalisha,
Komesha wako upudhi, za siri kutongolesha,
Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!

Twakujulia ubodhi, matendo ya kuchokesha,
Sipendelei maudhi, napenda ya kuridhisha,
Ihishimu yako hadhi, usizidi kukosesha,
Kidomodomo waudhi, kupayuka kwanongesha!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*