Mnaowachagua ni waroho, wafisadi na walio na ubinafsi. Wasiopenda wengine wakinufaika. Utatumia muda wako kwenda kuwachagua ila utabaki kulalamika tu. Ipo siku! Za Umma Zaharibiwa


Za Umma Zaharibiwa

Sijaona wamefaa, wabunge mnochaguwa,
Barazani watakaa, wanene kutambuliwa,
Watazamie kung’aa, ya umma kung’ang’aniwa,
Hata mkalia njaa, za umma yaharibiwa!

Mifukoni zinajaa, vema wakihudumiwa,
Wanaodhaniwa taa, mwanga umefunikiwa,
Kazi wameikataa, wakikosa cha kuliwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Njaa nayo yasambaa, wazalendo wanafiwa,
Kwingine wanapumbaa, wakata wamezidiwa,
Wafa bila kukomaa, pasi na kusaidiwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Za kondoo wamevaa, waja hamjagunduwa,
Maovu wanaandaa, vita haramu kuzuwa,
Waulize kuhadaa, viongozi watajuwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Wengine watanyamaa, hawataki jisumbuwa,
Wametuletea baa, hatari bila kujuwa,
Hawanalo la ridhaa, hawa tumewatambuwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Tunabaki kuzubaa, shida ni kujielewa,
Kwa wingi wana tamaa, watakazo hupatiwa,
Hutaka cha manufaa, kwa mengi wakisifiwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

© Kimani wa Mbogo (02/01/2011)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*