Tenda wema nenda zako! Wakisema, waache waseme. Jitie hamnazo! Usikose kutenda yako kwa sababu ya adui asiyekufaa wala asiyekulisha. Iwapo anacho kinyongo, mwache akajinyonge! Akajitie Kitanzi


Akajitie Kitanzi

Jukumu langu mwafaka, linipealo riziki,
Sisi tu wa moja rika, ya Maulana mabaki,
Kinyongo wamejitwika, wenyewe wanidhihaki,
Akionaye kinyongo, akajitie kitanzi.

Usinipuuze mimi, kinyongo usiwe nacho,
Mimi nimeshajihami, kwa silaha kochokocho,
Kwa uoga sisimami, ja kiguzo kifaacho,
Akionaye kinyongo, akajitie kitanzi.

Kinyongo ukijitwika, kajitwike peke yako,
Kokote nenda kuwika, nichomapo moyo wako,
Nenda kote hakahaka, kupoteza muda wako,
Akionaye kinyongo, akajitie kitanzi.

Sidindi kutenda wema, hata uone knyongo,
Mtaani sitahama, nihamapo niwe mwongo,
ukiona ninasema usiseme ni maringo,
Akionaye kinyongo, akajitie kitanzi.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2007)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*