Afya! Afya! Afya! Ni muhimu sana katika maisha ya binadamu. Mshairi hapa alitunga shairi la kumtakia afueni mzazi wake. Ni dhahiri kwamba, hata mshairi angekosa fedha, hangekosa maneno haya yaliyo na uzito mkubwa… Upate Afueni


Upate Afueni

Naichukua kalamu, nitunge na kuandika,
Malenga ninayo hamu, kheri kwa baba nataka,
Niandike la muhimu, vyomboni nilipeleke,
Natunga hili shairi, lichapishwe gazetini.

Lichapishwe gazetini, hadharani nilinene,
Baba haspitalini, naomba hima apone,
Huko Kenyatta jijini, kutoka tarehe nane,
Babangu yule mpendwa, Mola mkabidhi kheri.

Mola mkabidhi kheri, umnyoshee neema,
tupate njema habari, akiwa nafuu hima,
Nakusujudu Kahari, magotini nainama,
Nikumbuke babangu, nafuu kumtakia.

Nafuu kumtakia, aipate afueni,
Siku zinazowadia, afarijike moyoni,
Gazetini namwambia, atapata ahueni,
Aweze pona upesi, endapo ni kubwa bili.

Endapo ni kubwa bili, Mola fedha tupatie,
ninakuomba Jalali, hundi yako twandikie,
Kawatume wafadhili, wenyewe uwatumie,
Kishamponya babangu, mtima umfariji.

Mtima umfariji, kamjalie bashasha,
Dhabiti kama msaji, amalizapo kukwesha,
Wote wadhalilishaji, naomba waweze isha,
Kenyatta hospitali, nafuu nakutakia.

Nafuu nakutakia, dua naomba kwa jaha,
Neema nakutakia, upatapo ngema sifa,
Babangu nakwandikia, nikutakie furaha,
Uweze kupona hima, tumshukuru Karima.

Tumshukuru Karima, tumsujudu Jalali,
Shukrani twazituma, zende kwenu wafadhili,
Neema kuwaandama, tabibu hospitalini,
Abu pata afueni, kwetu nyumbani urudi.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2007)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*