Halibari ni mchafuko wa bahari. Kama halibari inavyowakumba wasafiri wa vyombo vya baharini, ndivyo mwanadamu hukumbwa na mengi maishani. Mengine yakiwa makubwa karibu kuzama. Halibari Baharini


Halibari Baharini

Twaeleya baharini, chombo juu ya mwamba,
Zote maili tisini, ndo bandarini kuramba,
Tuitiye nanga pwani, tucheleze tukiamba,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

Jahazi likatusomba, si tezini si ngamani,
Kaona pweza na kamba, kidukiza jahazini,
Mzubao katukumba, kuduwaa baharini,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

Maili katota ngamani, kwa turubali kusamba,
Wengi kaghumiwa ndani, baa belele kubamba,
Kimya kwao waloghani, katu hakuna kubemba,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

Walotuzonga ni mamba, kutizama baharini,
Walodukiza ni kamba, wakijikahiri ndani,
Wao wengi wa kujumba, kughumiwa kapteni,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

Sikitiko la tufani, wengi kadhani dumba,
Zilizala wakadhani, kwangu dua nikaomba,
Ya kiama wakadhani, kughofiriwa kaomba,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

Ni mengi yatatukumba, halibari maishani,
Yalo mengi tutaamba, kighumiwa kapteni,
Wana wa ndege tayumba, mti uendapo chini,
Halibari katukumba, baa tupu baharini.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2007)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*