Wapo walio na tabia za kujiona bora kuliko wengine. Watajidai wanavyojua ama wanayomiliki, lakini wapi? Maji yamezidi unga. Maji Yamezidi Unga


Maji Yamezidi Unga

Watetea kwa kuringa, husukutu mwafulani,
Wajiswifu ukilonga, wendako wabwaga zani,
Hujauona muwanga, umesalia kizani,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

Nyota yako umeshunga, ukasalia hunani,
Hujajuwa umewinga, sahibu jaha huoni,
Mali yote hujaanga, Ujione maskini,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

Wahadhiri zako kunga, za ndani hutowahini,
Ubozi umekuzonga, hujibaini mwandani,
Wajuzi wamekutenga, usalie u makani,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

Wonesha wako ujinga, kupungukiwa kichwani,
Mali yako ukiunga, fukara twakubaini,
Umeandamwa na janga, ukabakia mwambani,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

Ya moto imekudunga, una utungu mwilini,
Kiamboni hutotanga, kujiswifu hadharani,
Pindi ukiengaenga, utabaki huna peni,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

Matilaba hutogonga, itakwandama huzuni,
Vema hutotiya nanga, utoe yako maoni,
Shabaha hutoilenga, ukiambe cha thamani,
Maji yamezidi unga, sahibu huna hunani!

© Kimani wa Mbogo (01/01/2010)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*